KKKT waombwa kuwa wavumilivu
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP) limewataka washarika kutunza amani na umoja wa kanisa hilo wakati ikiendelea kufuatilia taarifa za askofu wa kanisa hilo, Dk. Alex Malasusa kukiuka mapatano yaliyotolewa na mkutano mkuu wa Maaskofu.
Katika taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Dayosisi Mashariki na Pwani , Godfrey na kusomwa jana katika Kanisa la Azania Front na Mchungaji Charles Mzinga imeeleza kuwa Dayosisi imetafakari kwa kina kuhusu jambo hilo na kujiridhisha kuwa halikuwa lengo la Dayosisi Mashariki na Pwani kupingana na maazimio ya mkutano wa maaskofu.
“Halmashauri inaendelea kulifuatilia jambo hili kwa makini. Washarika mnaombwa kuwa watulivu na kuliombea kanisa. Tunaombwa kutunza amani na umoja wa kanisa kama neno la Mungu linavyosema katika Waebrania 12:14,” Mchungaji Mzinga.
Dk Malasusa, Askofu wa Dayosisi ya Kusini Mashariki Lucas Mbedule na Dk Solomon Massangwa wa Dayosisi ya Kaskazini Kati wametengwa na wenzao wakituhumiwa kwa usaliti unaohusishwa na masuala ya kisiasa kwa kutosoma waraka wa pasaka.
Baraza la maaskofu wa KKKT katika mkutano uliofanyika Aprili 24 na 25 Jijini Arusha liliwapa muda wa hadi Septemba maaskofu hao kuandika barua kueleza kama wanaukubali au kuukataa waraka ambao walishiriki kuuandaa kwa ajili ya ujumbe wa Pasaka na iwapo hawatafanya hivyo hatua zaidi dhidi yao zitachukuliwa.
Hata hivyo tayari Askofu Mbedule alikwisha omba radhi na kueleza sababu za kutosomwa waraka huo ulitokana na sababu za kiusalama katika dayosisi kwamba haikuwa sawasawa ikiwa ni pamoja na migogoro ya ndani.
No comments
Post a Comment