Zahera katisha, amfunika Lwandamina
Umuhimu wa kocha huyo kwa kiasi kikubwa umeonekana katika safari ya Yanga nchini Algeria, ambako jana walikuwa uwanjani kumalizana na USM Alger.
KAMA kuna jambo la maana ambalo Yanga wamelifanya siku chache baada ya George Lwandamina kuwakimbia, basi ni kumchukua aliyekuwa Kocha Msaidizi wa DR Congo, Mwinyi Zahera.
Umuhimu wa kocha huyo kwa kiasi kikubwa umeonekana katika safari ya Yanga nchini Algeria, ambako jana walikuwa uwanjani kumalizana na USM Alger.
Yanga ilipotua tu uwanja wa ndege wa Algiers, maofisa wa uhamiaji uwanjani hapo walimzuia Zahera kutokana na kutokuwa na viza ya kuingilia hapa jambo lililoleta hofu, lakini kocha huyo kutokana na ujanja na ufahamu wake wa sheria za kimataifa alikwepa mtego huo.
Zahera alikwepa mtego huo baada ya kuwatolea ufafanuzi wa sheria inayoruhusu raia yeyote wa Ufaransa kuingia nchi nyingine ambayo ni koloni la Wafaransa bila viza, maelezo ambayo yaliwafanya maofisa hao kuduwaa na kusalimu amri mbele ya Mkongo huyo ambaye pia ni ana uraia wa Ufaransa.
Baada ya kufika hotelini, Yanga walianza kuumiza kichwa juu ya wapi watapata uwanja wa kufanyia mazoezi siku hiyo ndipo Zahera akafanya tena maujanja yake kwa kuwasiliana na rafiki zake pamoja na viongozi wa USM Algers ambao waliiruhusu Yanga kutumia uwanja wa wenyeji wao ambao, wamejificha nje ya jiji.
Mbali na hillo, Zahera kutokana na uwezo wake wa kuzungumza Kifaransa amekuwa msaada mkubwa kurahisisha mawasiliano dhidi ya wenyeji, maofisa wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), waamuzi na kamishna wa mchezo ambao wanazungumza lugha moja. “Napafahamu vyema Algeria, nina uzoefu na maisha ya huku, pia nina marafiki wengi huku ambao nimekuwa nikiwasiliana nao mara kwa mara na ndio maana unaona nimepazoea haraka,” alisema Zahera ambaye ameungana na Yanga ikiwa na mechi ngumu za Afrika.
No comments
Post a Comment