Sethi wa IPTL avuliwa madaraka
Aliyekuwa mmoja wa Wakurugenzi wa Kampuni ya IPTL, Harbinder Sing Sethi ameondolewa katika orodha ya wakurugenzi wa kampuni hiyo.
Uamuzi wa kumuondoa Seth katika ukurugenzi umefikiwa na bodi ya wakurugenzi ambayo pia imemvua madaraka ya kuwa mwenyekiti mtendaji wa IPTL, baada ya kushindwa kushiriki na kuhudhuria mikutano ya bodi.
Seth anadaiwa kushindwa kuhudhuria vikao vya bodi bila kuruhusiwa na wakurugenzi wenzake kwa miezi sita mfululizo tangu Juni 19, 2017 alipokamatwa na kushitakiwa.
Aidha, Mkutano huo ulikuwa na ajenda kuu ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili kampuni hiyo na uendeshaji wa mambo yanayohusu IPTL.
Sethi anakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababisha Serikali hasara ya Dola22.198 milioni za Marekani na Sh309.5 bilioni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kusutu.
“Bodi ilijadili kuhusu kesi namba 27 ya 2017 ya uhujumu uchumi inayomkabili ndugu Harbinder Sing Sethi na athari yake kwa kampuni, muundo wa kiutendaji wa kampuni ikiwemo na uongozi, udhibiti na ushushaji wa gharama pamoja na uwepo wa kesi mbalimbali mahakamani dhidi ya kampuni au ya kufunguliwa na kampuni,” amesema Lugenge.
Hata hivyo, katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari imesema kuwa bodi ilimtunuku Sethi ukurugenzi wa heshima kwa msingi kuwa aliongoza kampuni hiyo kutoka katika hatari ya kufilisiwa kutokana na kesi iliyokuwa imefunguliwa na kampuni ya VIP Engineering and Marketing kati ya mwaka 2002 hadi 2013.
No comments
Post a Comment