Shahidi atoa mpya mahakamani, aeleza anayedaiwa kuuawa yuko hai
Moshi. Mtuhumiwa wa mauaji ambaye ni shahidi wa nane wa utetezi, Muslim Mmbaga (35), jana aliwaacha hoi wasikilizaji katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, alipodai mtu anayedaiwa kumuua, yuko mitaani anatembea.
Mmbaga ambaye aliitwa kumtetea mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed, alidai marehemu Sebari Kitivo Mbura ni shahidi wa mashtaka katika kesi ya bilionea Erasto Msuya.
Shahidi huyo (Mmbaga) anayeshikiliwa katika Gereza la Karanga kwa kesi hiyo ya mauaji PI 206/2015, alitoa kauli hiyo wakati akihojiwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula baada ya kutoa ushahidi wake.
Wakili Chavula alimtaka shahidi huyo aieleze Mahakama, huyo marehemu anayetuhumiwa kumuua anaitwa nani, ndipo alipodai hajafa na ni miongoni mwa mashahidi wa kesi ya Msuya.
“Hakuna mtu aliyeuawa. Yuko hai na ni shahidi katika kesi hii. Ndiyo, anaitwa Sebari Kitivo Mbura yuko hai na yuko nje huru,” alidai shahidi huyo na kufanya wasilikizaji kuguna na kuangua kicheko.
Alidai kuwa awali, kesi hiyo ilikuwa ni ya unyang’anyi wa kutumia silaha uliotokea wilayani Same, lakini aliachiwa huru na Mahakama Mei 5, 2015 na akakamatwa tena na kushtakiwa kwa mauaji.
Alipoulizwa katika kesi hiyo alikuwa yeye na washtakiwa wangapi walioshtakiwa pamoja, Mmbaga alidai hakumbuki lakini baada ya kubanwa sana na wakili Chavula, akasema walikuwa washtakiwa watano.
Chavula alimuuliza kama anakumbuka namba ya kesi nyingine ya unyang’anyi wa kutumia silaha huko Siha, alidai hakumbuki hadi alipokumbushwa na wakili huyo kuwa ni CC 327/2014.
Alipoulizwa inakuwaje mambo yanayomhusu ya 2014 na 2015 hayakumbuki, lakini anakumbuka ya mwaka 2013 yanayomhusu Sharifu, shahidi huyo alidai ni kwa sababu anapenda vitu ‘vizuri vizuri.’
Akihojiwa na Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka na kutakiwa kueleza kama anavyomfahamu mke wa Sharifu kwa kuwa ni marafiki wakubwa, shahidi huyo alidai hamfahamu mke wa mshtakiwa.
“Mshtakiwa wa kwanza ni rafiki yangu sana. Namfahamu mtoto wake anaitwa Mohamed. Simjui mke wake kwa sababu siyo utaratibu mzuri kwa sisi Waislamu kumjua mke wa mwenzako,”alidai.
Awali, akitoa ushahidi wake kwa kuongozwa na wakili Hudson Ndusyepo, alidai anamfahamu mshtakiwa wa kwanza tangu mwaka 2009 na siku ya tukio la mauaji ya Msuya alikuwa naye Singida.
Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa ndani na nje ya Arusha, aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 7,2013 katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai.
Mmbaga alidai mwanzoni mwa Julai 2013, alikwenda katika machimbo ya dhahabu ya Londoni yaliyoko Ikungi Singida, baada ya kuona dhahabu inatoka, aliamua kumuita Sharifu kama rafiki yake.
“Tarehe 15.7.2013 Sharifu alinipigia simu kwenye saa 3 asubuhi akaniambia yuko njiani kuja Londoni na ilipofika saa 11 jioni alifika na nikampokea na kumpeleka kwa mwenyeji wangu,”alidai.
Mmbaga alidai kuwa siku iliyofuata walikwenda kuangalia maeneo ya migodi yenye dalili za kutoa madini mapema na kugundua dhahabu inapatikana ya kutosha katika machimbo hayo ya madini.
“Tuliendelea na shughuli hiyo mpaka tarehe 10.8.2013 majira ya jioni nilipoagana na Sharifu kwa vile alikuwa anarudi Arusha. Baada ya wiki moja nikawa nampigia simu akawa hapatikani,” alidai Mmbaga.
“Baada ya kupita wiki tatu kuna jamaa yangu wa Mirerani anaitwa Munisi akanipigia simu akaniambia jamaa yako (Sharifu) kakamatwa lakini hakuniambia amekamatwa kwa tuhuma gani.
“Nilitoka Londoni Oktoba na kurudi Arusha na nilipofika nikamtuma shemeji yangu anaitwa Magreth Mushi aende kumuona (Sharifu) gerezani. Aliporudi aliniambia Sharifu kasema niende mwenyewe.
“Nilikuja moja kwa moja mahakamani (akionyesha jengo lililoko nyuma yake), tukaonana akanieleza mkasa uliomkuta lakini nikamwambia asiwe na hofu kwa vile siku ya mauaji tulikuwa wote Londoni.”
Hata hivyo, alipoulizwa na Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka walikutana na Sharifu Mahakama gani, alisema ya Wilaya ya Moshi Mjini, ingawa aliyoionyesha kwa ishara ilikuwa Mahakama ya Mwanzo.
Shahidi wa saba wa utetezi
Awali, shahidi wa saba wa utetezi, Isack David ambaye ni mdogo wa mshtakiwa wa kwanza (Sharifu) aliieleza Mahakama namna mshtakiwa huyo, alivyokamata na polisi nyumbani kwake, Agosti 13,2013.
Shahidi huyo alidai kuwa baadhi ya vitu vya kaka yake vilichukuliwa na polisi zikiwamo bunduki zake mbili na vitabu vyake vya umiliki, pingu iliyokuwa nyumbani kwake pamoja na hati ya kusafiria.
Akiongozwa na wakili Ndusyepo kutoa ushahidi wake, shahidi huyo alidai siku hiyo alfajiri, alisikia mlango wa nje ukigongwa na alipotoka kwenda kufungua, alikutana na kaka yake sebuleni.
Shahidi huyo alidai mshtakiwa alimwambia aache akafungue yeye (Sharifu) kwa vile alikuwa amewaona kupitia kamera za usalama (CCTV), kuwa waliokuwa wanagonga walikuwa ni polisi.
Alidai, kabla ya siku hiyo, kaka yake alikuwa amesafiri kwenda Singida na siku hiyo hakuwa amefahamu kama alikuwa amesharejea hadi walipokutana sebuleni akitaka kwenda kufungua mlango.
Aliiambia Mahakama kuwa baada ya kaka yake kutoka nje, alibaki ndani ghorofani na akawa anachungulia dirishani, akaona magari mawili na yakaondoka na kaka yake.
Shahidi huyo alidai baada ya hapo, aliwasiliana na wazazi kuwaeleza hali halisi na walifika na kwenda Kituo cha Polisi Arusha na walipofika walijibiwa kuwa hakuna taarifa zozote za mtu anaitwa Sharifu.
Alidai kuwa baada ya hapo, alitoka na kuendelea na majukumu yake na siku iliyofuata saa tano asubuhi, alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha ni mkuu wa upelelezi Arusha.
David alidai kuwa mkuu huyo wa upelelezi ambaye hakumtaja kwa jina, alimtaka arudi nyumbani kwa kaka yake alipokuwa anaishi kwa kuwa wanataka kufanya upekuzi.
“Nilirudi nyumbani na nilipofika niliwakuta polisi ambao waliingia ndani na kuomba kuingia chumba cha Sharifu. Waliingia ndani ya chumba na kufanya upekuzi wa nyaraka zake mbalimbali.
“Baada ya upekuzi walichukua vitu ikiwamo bunduki yake kubwa na ndogo na vitabu vyake, Passport, DVR ya CCTV na pingu. DVR ilisharudishwa lakini sijui vitu vingine viko wapi,” alida David katika ushahidi huo.
Shahidi huyo ambaye alidai kuwa alikuwa akiishi na Sharifu kuanzia mwaka 2010, alikana kumfahamu Mussa na Adamu Leani.
Alipoulizwa kuhusiana na pikipiki mbili mpya zinazodaiwa kupelekwa nyumbani kwa Sharifu na kutumika katika mauaji, shahidi huyo alikanusha na kudai hazijawahi kupelekwa.
No comments
Post a Comment