Followers

Usiyaombee mataifa makubwa yapigane, yaombee yasipatane

Machi 4, 2018 kilizuka kizaazaa. Shushushu wa Uingereza, Sergei Skripal alipewa sumu akiwa na binti yake, Yulia Skripal, jijini Salisbury, England. Miili yao ilikutwa na kemikali za sumu zilizotengenezwa Urusi, aina ya Novichok nerve agent.

Ripoti ya madaktari kuhusu Skripal na binti yake kupewa sumu ya kemikali kutoka Urusi, ikawa sababu ya mvutano kati ya Uingereza na Urusi. Uingereza inaishutumu Urusi kutaka kumuua Skripal na bintiye. Urusi inajibu kuwa Uingereza inaichokonoa kwa kuizushia tuhuma zisizo na kichwa wala miguu.

Skripal na Yulia wamepona. Hata hivyo malumbano yakawa makali hadi kutoleana vitisho. Mgogoro wowote wa kidiplomasia unaoihusu Uingereza, na Marekani ipo. Urusi nayo haiwezi kuachwa na China.

Asili ya mgogoro wa Skripal ni uchokozi wa mataifa makubwa kufanyiana uvamizi wa kijasusi ili kudukua siri za ndani ya nchi. Skripal ni zao la ujasusi, kwani alikuwa jasusi wa Jeshi la Urusi kabla ya Uingereza kumgeuza ili awe anaichunguza Urusi na kuipa siri Uingereza.

Ndani ya taaluma ya ushushushu kuhusiana na upelelezi pamoja na ukusanyaji wa taarifa, jasusi anayetumika kumchunguza mwajiri wake na kuvujisha siri kwa nchi nyingine huitwa double agent. Hivyo, Skripal alikuwa double agent wa Uingereza.

Desemba 2004, Urusi ilimshutukia Skripal kwamba tayari alishakuwa double agent wa Uingereza, hivyo ilimburuza mahakamani ambako alihukumiwa kifungo cha miaka 13 jela. Mwaka 2010, Uingereza ilimkomboa Skripal kupitia makubaliano ya kubadilishana wafungwa wa kivita na ushushushu.

Ni dhahiri Urusi baada ya kumtoa Skripal kwa Uingereza haikuridhika, hivyo inadaiwa iliamua kumsaka imuue. Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May aliliambia Bunge (House of Commons) kuwa upelelezi umethibitisha bila kuacha shaka kwamba Urusi wanahusika na tukio la kumshambulia kwa sumu Skripal. Uingereza ulitafsiri tukio hilo kuwa ni uchokozi.

Jinsi Urusi ilivyojibu kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Sergey Lavrov, kwamba nchi yake ilikuwa tayari kwa lolote baada ya May katika hotuba yake bungeni Machi 12 na kuupa siku moja uongozi wa Rais Vladimir Putin uwe umeeleza walivyotekeleza shambulio la sumu, ndivyo shari ilivyoonekana dhahiri.

Vitisho vya pande mbili, vilisababisha kuwapo hisia za hofu kwamba huenda vita ingeibuka. Uingereza na Urusi kupigana ni jambo la kuogopa mno kwa usalama wa dunia kwa sababu lazima mataifa yote makubwa yataingia. Hapo ni kumaanisha China na Marekani hazitokaa kando. Uingereza pia ni mwanahisa mwenye nguvu kwenye Jeshi la Kujihami la Nchi za Magharibi (Nato).

Hofu kubwa inaletwa na nadharia ya dola moja kuongoza nyingine kisiasa, kiuchumi na kijeshi. China, Urusi na Marekani ndiyo wanaopambana hivi sasa kujisimika ukiranja wa dunia kiuchumi, kisiasa na kijeshi. Hiyo ndiyo sababu wanapelelezana na kudukuana.

Marekani ilipofanya uchaguzi Novemba mwaka juzi, China na Urusi hawakulala. Ilikuwa muhimu mno kwao kwa ushindi wa kiongozi mwenye sura zenye kupunguza mabavu ya Marekani duniani.

Hii ni sababu vyombo vya usalama vya Marekani vilikuwa vikali sana baada ya kubaini kuwa Urusi iliwafanyia udukuzi kwenye uchaguzi wa mwaka jana, hivyo kuchangia ushindi wa Rais Donald Trump.

Urusi inarejea upya kupitia Shirikisho la Urusi baada ya anguko la dola ya Umoja wa Nchi za Kisovieti (USSR) mwanzoni mwa miaka ya 1990. Nayo ina maumivu yake kwa sababu Marekani ndiyo iliyoiandama Sovieti na kuchochea nchi za USSR kujitenga na umoja huo.

Marekani na Urusi ni nchi zenye kisasi. Urusi inaamini kuwa kama USSR isingeanguka, maana yake ubabe wa Marekani leo usingekuwapo. Marekani haitaki Urusi irejee nguvu zake za Sovieti. Urusi inatambua kuwa palipo na Marekani kuna Uingereza.

Wakati huohuo ukubwa wa China, watu wengi ilionao, ustawi wake wa kiuchumi kupitia sera zake za Kikomunisti na jinsi inavyojitandaza duniani, ni sababu ya Marekani kukosa usingizi.

Katika eneo la uchumi, Urusi inaachwa nyuma na ushindani unaonekana kati ya China na Marekani. Kijeshi mataifa yote hayo yapo imara na kwenye siasa tayari Urusi imeshaonekana tishio.

Mataifa yote hayo yana uchokozi. Yametengeneza mashushushu ambao wamesambaa ulimwenguni kote.

Tabia ya China kuwa rafiki wa mataifa madogo kisha kutengeneza urafiki uliokomaa, imeifanya nchi hiyo kuwa na mtandao mpana wa kiuchumi duniani. Hali hiyo iliishtua Marekani, nayo ikaamua kujishusha ili kutengeneza ushirikiano mpana na mataifa madogo.

Ndiyo maana China na Urusi wamekuwa na furaha kwa ushindi wa Trump kwa sababu wanaamini kiongozi huyo hatataka kujishusha kama walivyokuwa marais watatu waliomtangulia – Barack Obama, George Bush na Bill Clinton.

Ingekuwa pigo kubwa kwa China na Urusi kama Hillary Clinton angeshinda kwa sababu tayari alishakuwa na uelekeo wa kutengeneza ushirika mpana wa kiuchimi kwa nchi ndogo.

Imani yao ni kuwa miaka minne, zaidi ikiwa nane ya urais wa Trump, ni mingi na inatosha kuvuruga nguvu ya Marekani kisha wao kujisimika na kujitanua. Ndiyo maana vigogo wa Marekani, wenye kujua hili hawakumtaka na wanaendelea kutomtaka Trump.

Wanafahamu kuwa ulimwengu wa sasa huwezi kuitawala dunia kwa mtindo wa Adolf Hitler. Dunia ya sasa inataka taifa imara lishuke na kujigeuza msaada kwa mataifa madogo. Jinsi taifa kubwa linavyosaidia nchi ndogo ndivyo linavyoingia ndani na kujisimika.

Afrika ya leo ni mtumiaji mkubwa wa bidhaa kutoka China, hilo halikutokea mara moja. Kuna maandalizi makubwa yalifanyika. China ni mzalishaji, kwa hiyo uimara wake unategemea zaidi soko katika nchi ambazo huzisaidia.

Nchi zote hizo zinamiliki silaha za nyuklia, kwa hiyo hakuna ambayo ina unyonge kwa mwenzake.

Kwa ubabe kabisa, Rais wa Marekani kila anapokuwa pembeni yake kuna askari aliyebeba mkoba mweusi. Mkoba huo ndani yake huwa na kitu mfano wa laptop, kinaitwa Nuclear Football.

Hiyo Nuclear Football ni rimoti ambayo Rais wa Marekani popote anapokuwa anaweza kuilipua nchi yoyote aitakayo kwa kutumia alama yake ya kidole. Kwa mantiki hiyo, Marekani wametega nyuklia kuelekea nchi yoyote duniani. Ni suala la Rais wa kubonyeza kidole kwenye Nuclear Football.

Mkoba wa nyuklia wa Urusi unaitwa Cheget ambao Rais wa Urusi muda wote yupo nao pembeni. Kama akitaka kulipua nchi yoyote ni suala la kufungua mkoba na kuchagua sehemu ya kuelekeza shambulio. Watu wengine wenye dhima ya kutunza Cheget ni waziri wa ulinzi na mnadhimu wa jeshi.

Upande wa China imekuwa na siri kubwa kuhusu mamlaka ya ulipuaji wa mitambo yao ya nyuklia, ingawa ipo dhana kuwa Rais na Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti, anayo mikoba yenye mashine za ulipuaji ila wanafanya siri.

Kuhusu silaha, mataifa hayo yanaendelea na ushari wao. Marekani wanamiliki ndege za Stealth Fighters ambazo zimetengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu kiasi kwamba zinaweza kuvuka anga yoyote pasipo kuonekana na rada za nchi husika. Ndege hizo zipo za aina mbili, 187 F-22s na F-35.

China na Urusi nazo zipo kamili. China ina aina nne ya Stealth Fighters, ambazo ni J-31, J-20, F-35 na F-22. Urusi wao wana aina moja tu ya Stealth Fighters ambayo ni F-22. Aina nyingine ambayo itakuwa ya pili kwa Urusi ni T-50 ambayo bado hazijazinduliwa.

Mataifa hayo yanamiliki vifaru vizito zaidi vya kivita, manowari pamoja na meli. Zipo pia ndege zisizo na marubani.

Uingereza pia wana nyuklia, ingawa ipo siri kubwa kuhusu mkoba wa kufyatulia mitambo ya nyuklia. Inaaminika kuwa ama Waziri Mkuu au Waziri wa Ulinzi, mmoja ndiye mwenye rimoti. Hivyo, ugomvi na nchi hizo, huweza kusababisha matumizi ya nyuklia, hivyo kuipa dunia msukosuko mkubwa.

Mataifa yenye kuwania ukiranja wa dunia hayapaswi kupatana ila yasigombane. Leo hii Korea Kaskazini ipo salama kwa sababu wakubwa wanavutana. Marekani inatamani kuinyuka lakini inahofia China na Urusi.

Kama wakubwa wangekuwa wanapatana leo, Bashar al-Assad angekuwa ameshang’oka Syria, Kim Jong-un asingekuwa mtawala wa Korea Kaskazini.

Wababe wa dunia hawataki kuharibu mitambo yao ya silaha za nyuklia lakini pia hawataki na wengine wamiliki silaha za maangamizi kama wao. Kwa kujipendelea, Julai Mosi, 1968, mataifa makubwa yalisaini mkataba wa kuzuia kusambaa kwa utengenezaji wa silaha za nyuklia ulioanza kutumika Machi 5, 1970.

Kama mataifa makubwa yangekuwa na dhamira ya kutokomeza nyuklia hasa baada ya kuona athari zake kwenye Vita Kuu ya Pili ya Dunia, mkataba huo ungehusu kutokomeza nyuklia na siyo kuzuia ongezeko.

Kuzuia ongezeko kulimaanisha waliokuwa na silaha hizo mpaka Machi 5, 1970, waendelee kuwa nazo na wale ambao hawakuwa nayo wasiwe na uwezo wa kumiliki.

Kutokana na nguvu kubwa ya kijeshi na silaha ambazo mataifa makubwa yanamiliki ni suala la kuombea wasije kupigana wao kwa wao, itakuwa hatari kwa usalama wa dunia.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.