Followers

‘Ukinyonga’ katika siasa ni mbaya kwa vijana


Unapomzungumzia kijana anayetaka kuiletea mabadiliko nchi yake kupitia siasa, bila shaka utamkumbuka Mwafrika wa kwanza kutunukiwa Shahada ya Uzamivu, William Dubois.

Dubois hakutaka kuitumia sifa ya kuwa Mwafrika wa kwanza kupata PhD kuchumia tumbo, bali aliitumia kisiasa kwa kuamini huko ndiko kwenye ukombozi wa kweli.

Aliitumia elimu hiyo kudai haki za mtu mweusi nchini Marekani, katika kampeni maarufu iliyokuwa ikijulikana kama “Back To Africa”.

Kupitia kampeni hii wapo Wamarekani waliorudi Afrika kutafuta asili zao na wapo walioamua kubaki huko huko.

Hapa nchini wanasiasa vijana ni wengi, lakini kwa bahati mbaya wengi wao wamegubikwa na ugonjwa wa kuchumia tumbo, hata wale waliokuwa na elimu badala ya kuzitumia kuleta manufaa katika jamii kupitia siasa, pia wameitumia kujinufaisha wao binafsi.

Wanasiasa wasomi ndiyo walitegemewa sana kuibua mijadala yenye tija hususani ya kimaendeleo kwa sababu wana elimu na pengine wana nafasi nzuri ya kujua vitu vingi kupitia elimu walizonazo.

Changamoto hii isipoangaliwa na vijana wenyewe wakati huu, kuna hatari ya kuzalisha wanasiasa wasiokuwa na misimamo katika vizazi vijavyo kutokana na kuiga kutoka kwa waliowatangulia.

Ukada, ushabiki wa vyama kindakindaki hutawala vichwa vya vijana walio wengi tofauti na uhalisia na namna wanavyopaswa kufikiri juu ya mustakabali wa siasa za nchi.

Kelele za kudai demokrasia zinapaswa kwendana na mawazo chanya badala ya kugandamizwa na ukanda unaosababisha kusahau mambo ya msingi na kujikuta ni vinyonga katika siasa.

Ndiyo vijana wengi ni vinyonga katika siasa, licha ya kuwapo kwa vuguvugu la vijana kutamani kuingia katika mbio hizo.

Ninasema, tena kwa kujiamini kuwa vijana wa Tanzania bado hawajaitendea haki siasa kutokana na wengi wao kutokua na misimamo.

Miongoni mwa sifa za kiongozi bora, mwanasiasa bora ni kutoyumba katika kile anachokiamini, hususani katika maamuzi yake binafsi.

Lakini linapokuja suala la siasa ambalo kwa namna yoyote ile linagusa mambo muhimu ya nchi ndiyo shaka inakuwa kubwa anapoonekana au kusikika kijana aliyejiita mwanasiasa halafu anayumba katika maamuzi.

Wengi wao wanapoyumba au kuingia katika kundi la wachumia tumbo hawakosi sababu, ila yote kwa yote hubainika kuwa njaa inawasumbua.

Baadhi yao wameaminiwa na kada wanazoziongoza, lakini kwa sababu moja ama nyingine wameutia shaka uongozi wao kutokana na maamuzi yao nasisitiza wamekuwa vinyonga na kudiriki kunyonga siasa wanayojinasibu kuitumikia na kuipenda.

Wamekuwa wakifanya mambo mengi yanayowafanya kuwa wanasiasa uchwara kwa kukubali kutumiwa na wanasiasa wakongwe au kujiingiza katika mambo yasiyopaswa kufanywa na mwanasiasa aliyekomaa ikiwamo vurugu, utovu wa nidhamu, uropokaji majukwaani kwa kisingizo cha kuhubiri siasa.

Fikra za walio wengi ni kwamba vijana wana wajibu wa kufanya siasa. Ukakasi unabaki pale pale walio wengi wanaingia kwa mkumbo au kwa sababu batili nilizozitaja hapo juu na kubaki katika kundi la wasiojitambua na hawajui siasa za Tanzania zilipotoka na wapi zilipo.

Natamani siku moja wanasiasa vijana wote wakaamini siasa ni kujenga hoja, kuzitetea kwa ajili ya kuleta maendeleo ya taifa, badala ya kuwa bendera fuata upepo na kuyumba kila upande ilimradi kuna harufu ya ulaji.

Ni wajibu wa kijana kufanya siasa, hususani wasomi ili kuwa na wigo mpana wa kujadili na kuchambua mambo, wajibu ulio mkuu kwao ni kujipanga kutokuwa kinyonga wa kisiasa kabla ya kuingia kwenye siasa.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.