Mzazi Jijengee Utaratibu Huu Kwa Wanao Ili Kuleta Kizazi Chenye Tija
Ewe mzazi mwezangu, najua una majukumu mengi katika sayari hii, ila nakuomba usome hili ambalo lipo katika makala haya, kwani ni la muhimu sana zaidi ya hata uzaniavyo. Lengo la kuandika walaka huu ni kwamba mara kwa mara macho yangu yamekuwa yakiona tabia hii ikizidi kukithiri kwa wazazi wengi.
Wazazi wengi tumekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wetu wanapata huduma zote zile za msingi. Tumekuwa tukihakikisha watoto zetu wanapata elimu, chakula pamoja malazi , halikadharika na afya bora. Katika hili niwapongeze wale wote ambao huwa wanalitimiza hili hili kwa moyo wote pasipo kupindisha shingo.
Lakini pamoja na kuendelea kuwapa mahitaji hayo ya msingi, wengi wetu tumesahau ya kwamba watoto wetu wanahitaji mambo mengine mbali na hayo niliyoaanisha hapo juu. Wengi wetu tumekuwa tupo bize na utafutaji wa fedha muda mwingi, kuliko kukaa na familia zetu husasani watoto zetu.
Wapo baadhi ya wazazi nimekuwa nikiwasikia wakisema wapo bize katika kuhakikisha wanatafuta ugali wa watoto, wamekuwa wakitoka majumbani mwao muda wa asubuhi ambapo hata watoto hao wanakuwa bado wamelala, Hata muda wa kurudi nyumbani wamekuwa wakichekewa, na kukuta watoto wamekwisha lala, na tabia hii huenda ukaona mzazi upo sawa, lakini ukweli unakosea sana.
Kwa mtindo huu unadhani haya ndiyo malezi bora kwa mtoto? Bila shaka kama wewe ni mmoja wa mzazi mwenye tabia kama hii ni vyema ukatafakari na kuona jukumu lako kama mzazi ni lipi? Na madhara ya kufanya hivyo ni yapi?
Kwani binafsi naamini mtoto kama mtoto anahitaji muda wa kuweza kubadilishana mawazo pamoja na mzazi wake achilia mbali na marafiki zake. Kwani katika dunia hii kumekuwa na mambo mengi ambayo yamekuwa si mazuri na mengine ni mazuri. Na kwa kuwa mtoto hapati muda wa kukaa na wazazi wake ili wamueleze yapi ni mazuri na yapi ni mabaya, mtoto amekuwa akiyatenda yote kwa sababu amekuwa haoni uhimizo wowote kutoka kwa wazazi wake.
Kwa kufanya hivyo wazazi wamekuwa wanashtuka dakika za mwisho mambo yakiwa yamekwisha kuharibika kabisa, na wazazi hao hao mwisho wa siku huwanyoshea vidole watoto hao na kusema ya kwamba wameharibika na hawafai. Huku wamesahau wazazi hao ndiyo chanzo cha kumomonyoka kwa maandili kwa watoto hao, na hii ni kwa sababu wazazi wamekuwa wakijitenga na jukumu la kufuatilia mienendo na tabia za watoto hao kiujumla.
Hivyo ni jukumu la kila mzazi kutenga muda walau hata kwa wiki mara tatu kuweza kuzungumza na mwanae elimu zote za afya, jamii, mahusiano na elimu zinginezo. Wazazi wengi wamekuwa wakiona aibu kutoa elimu hizo kwa watoto zao, huku wakiamini kufanya hivyo ni sawa nakwenda kinyume na maadili.
Lakini ukweli ni kwamba mzazi una jukumu la kumuelimisha mwanao mambo yote. Pia ewe mzazi ukumbuke ule usemi usemao ”kukonda kwa mbwa si aibu kwa mbwa bali ni kwa mfuga mbwa”.
Mwanao akajiingiza katika makundi mabaya yaliyopo hivi sasa aibu haitakuwa kwa mwanao bali itakuwa ni aibu ya kwako mzazi. Hivyo mzazi mwenzangu ni heri ukawajibika kila sekta katika kuhakikisha watoto wako unawaelea katika misingi inayoelewa, kwani pindi utakaposhindwa kuwalea watoto zako, dunia hii ipo kwa ajili ya kuwafunza wale wote ambao wameshindwa kufunzwa na mamaye.
No comments
Post a Comment