Aishi Manula? Beno Kakolanya? Ngoja nikwambie kitu
Na Tom Thomas
Beno Kakolanya. Baada ya mechi Simba na Yanga kila mtu alilitamka jina lake, hata wale waliokua hawamfahamu vizuri walilitaja jina lake kwa heshima. Ndio, baada ya ile kazi kubwa aliyoifanya
alistahili heshima.
Alikua kwenye kiwango bora sana, kama isingekua ubora wake pale golini mambo yangekua tofauti sana. Pengine tungekua tunamsifu mchezaji mwingine tofauti na yeye.
Huu ni msimu wa tatu akiwa Yanga. Alisajiliwa baada ya kuwa na msimu mzuri akiwa Prisons FC ya Mbeya. Aliwakuta Ali Mustapha na Deogratius Munishi wakiwa kwenye viwango vya kupanda na kushuka. Kuna wakati Ali Mustapha alionekana kuwa bora kuna wakati Munishi alionekana kuwa bora.
Ilionekana ni ngumu kwa Kakolanya kupata nafasi. Ali Mustapha na Munishi walikua wakibadilishana.
Ndivyo ilivyokua. Hakupata nafasi kubwa ya kucheza.
Hata baada ya Munishi na Ali Mustapha kuondoka bado ilikua ni ngumu kwa Beno kuaminika. Aliletwa
Youthe Rostand na bwana'mdogo Ramadhani Kabwili. Bado hakuaminika sana. Alikua akipata nafasi ndogo. Ingawaje kuna wakati majeraha yaliathiri sana nafasi yake.
Mvumilivu hula mbivu. Yawezekana Beno aliishi kwenye usemi huu. Yawezekana aliamini ipo siku
ataheshimika na kukubalika. Jina lake litajwa kwa heshima kubwa. Kama ilivyo sasa. Kitu kizuri ni
kwamba alifanya vizuri kwenye mechi kubwa, mechi inayotazamwa zaidi. Ni kama vile alivyofanya Manyika Jr mechi ya mwaka 2014.
Kwenye soka letu ili uonekane na kukubalika zaidi ni lazima uoneshe uwezo mechi ya Simba na Yanga
au mechi yeyote dhidi ya Simba au Yanga. Hapo utafahamika sana.
Unamkumbuka Said Bahanuzi? Alifunga goli mechi moja ya Simba na Yanga ghafla akawa mkubwa
sana. Davis Mwape alifunga goli mwaka 2011 akakubalika. Kenneth Asamoah na Malimi Busungu
walipata umaarufu baada ya kufunga goli kwenye mechi hizi.
Jerryson Tegete alipendwa kwa sababu ya kuifunga Simba kama iliyokua kwa Mussa Mgosi kuifunga
Yanga. Shiza Kichuya amekua akisifika kutokana na kufanya vizuri kwenye mechi hizi.
Beno Kakolanya kwa sasa yupo kwenye kiwango kizuri, ni mmoja kati ya magolikipa wenye uwezo mkubwa. Haitashangaza kama kocha Mwinyi Zahera atampanga yeye dhidi ya Klaus Kindoki, golikipa wa kimataifa kutoka Congo.
Achana na Beno Kakolanya. Kwa takribani miaka mitano sasa Aishi Manula ndiye golikipa namba moja
nchini. Tayari kuna mjadala wa nani anayestahili kuwa golikipa namba moja wa Tanzania kati ya Aishi
na Beno.
Kuna wakati alikuja Hussein Shariff 'Casillas' alikua bora sana. Kuna wakati alikuja Shaban Kado akafanya vizuri sana. Hawa wote wakuweza kufanya vizuri na kumuondoa Aishi. Hawakuweza kuwa bora kwa miaka iliyoendelea. Sasa amekuja Beno.
Kwa miaka mingi tumekua na tatizo la kutotengeneza magolikipa wazuri walio na muendelezo wa kiwango bora. Wengi tunaowapata ni wale wanaofanya vizuri ndani ya miaka miwili mitatu kisha wanapotea. Kama ilivyokua kwa Mwadini Ali.
Sasa amekuja Beno. Anaonekana kuwa golikipa mzuri sana. Inabidi ajifunze kilichowakwamisha kina Mwadini, Husein 'Casillas' na Kado ili endelee kuwa bora kwa miaka mingi inayokuja.
Ngoja nikwambie kitu. Unapokua na magolikipa wawili walio wenye ubora ni faida kubwa kwa nchi. Kocha anakua na uwanja mpana wa kuchagua nani ampange kwenye kikosi. Na hata mmoja wao anapokosekana timu haiathiriki sana. Huu si wakati wa kuanza kutafuta nani ni bora kati ya Aishi na Beno.
Ni wakati wa kufarijika na kufurahi kwamba Tanzania inatengeneza wachezaji wazuri. Wachezaji wanaoweza kuiletea faida nchi. Wakati wa kufarijika kwamba Aishi anapata changamoto nzuri kwenye nafasi yake. Kwa sasa, hata Aishi anapokosekana kuna faraja ya uwepo wa Beno.
Tatizo linaweza kuwa ni sisi wenyewe. Yawezekana kuna siku Aishi atafanya kosa basi kelele zitakua kwanini Beno hapagwi. Beno anaweza fanya kosa akalalamikiwa kocha kwa kutompanga Aishi. Ndivyo soka letu lilivyo. Tunasahau kama mpira ni mchezo wa makosa.
Huu ni muda wa kumuacha kocha wetu Emmanuel Amunike afanye kazi. Bado tuna nafasi kuelekea Afcon, kama tutafanya vizuri kwenye mechi tatu zilizobaki. Si muda wa kuanza kutafuta nani bora kati ya Aishi na Beno. Ni muda wa kushirikiana ili Taifa stars yetu ifanye vizuri.
0754 896963
No comments
Post a Comment