Ugonjwa wa mafua, chanzo, dalili na matibabu yake.Ugonjwa wa mafua, chanzo, dalili na matibabu yake.
Ugonjwa wa mafua unaweza kusababisha hali ya kupiga chafya mara kwa mara, kutokwa na makamasi mepesi au mazito puani, kikohozi, homa kali, na kuziba kwa pua.
Dalili hizi huanza ndani ya saa 16 tokea wakati wa kugusana na virusi au visababishi vya mafua. Na hali huwa mbaya katika kipindi cha saa 24 hadi 72 ambapo virusi huwa vingi katika majimaji yatokayo puani.
Katika kipindi hiki mgonjwa wa mafua huwa na uwezo mkubwa wa kuambukiza watu wengine. Dalili za ugonjwa wa mafua hutegemea zaidi uwezo wa mwili wa kupambana na magonjwa kuliko uwezo wa virusi kushambulia nyama za mwili katika njia ya mfumo wa hewa.
Mafua yanaweza kusababisha matatizo makubwa katika mfumo wa kupumua hasa pale yanapoambatana na uambukizo wa pili wa bakteria. Matatizo yanaweza kuwa makubwa zaidi kwa watoto wachanga, wazee au kwa watu wenye upungufu wa kinga mwilini.
Mafua pia yanaweza kusababisha ugonjwa wa uambukizo wa bakteria katika matundu ya fuvu la kichwa (sinusitis), uambukizo katika masikio na koo.
Na katika kipindi hiki mgonjwa hutoa makohozi au makamasi yenye rangi ya njano yanayofanana na usaha. Katika hatua hii, mgonjwa wa mafua anaweza kupata homa kali sawa na mtu mwenye homa ya Malaria.
Kimsingi mafua yanasababishwa na uambukizo wa virusi vya mafua. Wataalamu wa maswala ya afya na tiba wanasema kuwa, kuna aina zaidi ya 200 za virusi vinavyosababisha mafua ingawa virusi aina ya rhinoviruses vilivyogunduliwa miaka ya 1950, ndivyo vinasababisha mafua kwa kwa asilimia 30 hadi 80.
Aina zingine za virusi vya mafua ni human coronavirus, influenza viruses, adenoviruses, human parainfluenza viruses, human respiratory syncytial virus, enteroviruses na metapneumovirus.
Mara nyingi mtu anaweza kupata uambukizo wa virusi vya mafua vya aina mbalimbali kwa kipindi kimoja anapoumwa mafua.
Kwa kawaida mafua hutokea zaidi wakati wa mvua na baridi kali. Hii ni kutokana na uwezo wa virusi wa mafua kusambaa kwa kasi wakati wa baridi. Lakini pia katika kipindi cha baridi kali njia ya hewa katika mfumo wa kupumua, huwa kavu kiasi cha kushindwa kukabiliana na virusi wa mafua kwa ufanisi mkubwa.
Mafua pia yanaweza kusababishwa na mzio katika mfumo wa kupumua. Utafiti uliofanywa katika hospitali ya Bugando jijini Mwanza, ulionyesha kuwa mafua yatokanayo na mzio katika mfumo wa kupumua huchangia kwa asilimia 14.7 katika mzigo wa wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo kutokana na magonjwa ya mfumo wa kupumua.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Said A. Said kwa kushirikiana na Mabula D. Mchembe, Phillipo L. Chalya, Peter Rambau pamoja na Japhet M. Gilyoma na kuchapishwa katika jarida la mambo ya tiba la magonjwa ya hewa, BMC Ear, Nose and Throat Disorders.
Tafiti mbalimbali za afya ya jamii pia zinaonesha kuwa, mafua yatokanayo na mzio wa njia ya kupumua ni tatizo la ulimwengu mzima na kwamba utokeaji wa tatizo hili ni asilimia 10 hadi 40 na tatizo hili linaongezeka.
Sababu kubwa zinazochangia kutokea kwa aina hii ya mafua ni uchafuzi wa hewa, vumbi hasa la ndani ya nyumba, moshi wa sigara, hali ya baridi na matumizi ya pafyumu zenye harufu kali.
Kwa kawaida mafua yatokanayo na mzio hayaambatani na homa, yanakuwa meupe, mepesi, wakati mwingine yanaambatana na muwasho wa macho, ugonjwa wa pumu au kutokea kwa uvimbe wa vinyama puani (nasal polyps).
Katika utafiti ulioongozwa na Zitta J na kuchapishwa katika jarida la Chama cha Madaktari cha Marekani (AMA) toleo la 288(23), ilibainika kuwa watu wanaosafiri kwa ndege kwa muda mrefu kuanzia saa moja na kuendelea, wana uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa wa mafua.
Sababu ya jambo hili kwa mujibu wa utafiti huo ni kwamba, kinga ya miili ya abiria wa ndege dhidi ya mafua (mucociliary clearance system) huparaganyika kutokana na ukavu wa hewa ndani ya ndege. Unyevu wa hewa katika ndege inayosafiri zaidi ya saa moja hupungua kufikia kiasi cha asilimia 10 hadi 5.
Ukavu wa hewa au kupungua kwa unyevu katika hewa, husababisha vinywele (cilia) katika njia ya hewa kushindwa kukamata virusi vya mafua na kuvisafirisha hadi tumboni ambako kwa kawaida huunguzwa kwa tindikali (acid) ya tumboni na kufa. Mwili wa binadamu hufurahia na kuwa katika hali bora pale unyevu wa hewa unapokuwa kati ya asilimia 20 na 60.
Njia zinazosaidia kukabiliana na tatizo la mafua ni pamoja na kunawa mikono mara kwa mara na kuepuka kushika shika pua na macho. Ni vizuri kufunika pua na mdomo kwa kitambaa wakati wa kupiga chafya.
Katika utafiti wao wataalamu wa Chuo kikuu cha Carnegie Mellon waligundua kuwa watu wenye telomere ndefu katika vinasaba vya seli zao aina ya CD8CD28, wana uwezo mkubwa wa kudhibiti virusi vinavyosababisha mafua.
Utafiti huo uliongozwa na Shaldon Cohen na kuchapishwa katika jarida la Chama cha Madaktari wa Marekani (JAMA), Februari 2013.
Tafiti kadhaa pia zinaonyesha kuwa watu wanaofanya mazoezi ya mwili mara kwa mara, hawakabiliwi na tatizo la mafua mara nyingi ikilinganishwa na wale wasiofanya mazoezi. Hali hii yaweza kusababishwa na kurefuka kwa telomere kwa sababu ya mazoezi.
Kula mbogamboga na matunda kwa wingi pia ni njia bora ya kupunguza uwezekano wa kupata mafua mara kwa kutokana na kupata vitamin C na madini ya zinki kwa wingi katika vyakula hivi.
Vitamini C na zinki husaidia kinga ya mwili kukabiliana na virusi mbalimbali na kupunguza hatari ya kupata mzio utokanao na vyakula vya asili ya wanyama.
Mtaalamu wa sayansi ya tiba ya akili (Neuropsychologist) Dk David Lewis, katika utafiti wake aligundua kuwa furaha na kicheko cha mara kwa mara, husaidia katika kukabiliana na tatizo la mafua.
Dk Lewis anasema kuwa utafiti wake ulihusisha wagonjwa wenye mafua kuangalia vipindi vya futuhi (comedy) na baada ya dakika 30, zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa walipata nafuu. Hii ni kwa mujibu wa Tom Morgan kama ilivyoandikwa katika mtandao wa www.express.co.uk mnano Januari 24, 2014.
No comments
Post a Comment