Naibu Waziri awataka Wakandarasi waliohusika na miradi ya Maji Karatu ndani ya Siku 14
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amemtaka mkuu wa wilaya ya Karatu kuwatafuta wataalam wa serikali, pamoja na wakandarasi waliopata zabuni za kutekeleza miradi ya maji wilayani Karatu kufika wilayani hapo bila kukosa ndani baada ya siku 14. Wito huo ni kuanzia Tarehe 28 Januari, 2019 ili kufanyika kikao na wahusika kueleza jinsi walivyosimamia na kutekeleza miradi ya maji wilayani Karatu.
Naibu Waziri huyo amesema katika kikao hicho asitumwe mwakilishi, bali wahusika wenyewe, na atashiriki kikao hicho ili kubaini changamoto zote za miradi ya maji wilayani Karatu na kutafuta jibu ili maji safi na salama yawafikie wananchi na wadau wengine kwa wakati kama serikali ilivyopanga.
Waziri Aweso katika ziara ya ukaguzi amesema imebainika baadhi ya miradi ya maji imekabidhiwa ikiwa na mapungufu na makosa mbalimbali hali ambayo haikubaliki, pia kutowatendea haki wananchi wanaohitaji maji kwa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Awali, Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Theresia Mahongo amesema kuwa miongoni mwa changamoto za miradi ya maji wilayani hapo ni mapungufu ya kiusanifu. Amesema hali hiyo imetokana na miradi ilipoanza kutekelezwa mwaka 2012/2013 haikufanyiwa mapitio ya usanifu upya baada ya mtaalam mshauri kampuni ya Tanplanet Njegimi Express kuachishwa kazi kwa kutokidhi viwango.
Halmashauri ya wilaya ya Karatu ilipangiwa kutekeleza miradi ya maji katika vijiji 10 na katika halmashauri hiyo miradi ilipangwa kuhudumia vijiji 13 kwa kutekelezwa katika vijiji vya Getamock/Mahhahha, Khusumay, Kansay, Buger, Endonyawet, Matala, Endamaghang/Mikocheni, Laja/Umbangw, Mang’ola Juu na Makhoromba.
No comments
Post a Comment