Followers

Uchaguzi DRC: Polisi wapelekwa katika ofisi za Tume ya Uchaguzi, upinzani washinikiza matokeo yatangazwe

Polisi wamekita kambi mbele ya majengo ya makao makuu ya Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Ceni) huku mustakabali wa lini matokeo yatatangazwa ukiwa bado shakani.

Mwandishi wa BBC Swahili jijini Kinshasa, Mbelechi Msoshi ameshuhudia magari yaliyosheheni polisi mbele ya ofisi za Ceni na anaripoti kuwa vizuizi vya barabarani vimewkwa . Hakuna mtu wala magari yanayoruhusiwa kukatisha mbele ya ofisi hizo.

Watu tayari wameshaanza kuondoka kwenye maeneo ya karibu na jengo hilo na kuna taarifa zisizo rasmi zinazoeleza kuwa huenda matokeo yakatangazwa baadae leo ama kesho.

Mgombea wa urais wa upinzani Martin Fayulu jana Jumanne aliwaonya maafisa wa uchaguzi dhidi ya kile alichokiita "kuficha ukweli".

Bwana Fayulu amesema "watu wa Congo tayari wanajua "matokeo ya uchaguzi uliyofanyika Desemba 30."

"Tume ya uchaguzi (Ceni) lazima itangaze matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais hivi karibuni. Matokeo ya uchaguzi kamwe hayana mjadala."

Matokeo ya awali ya uchaguzi huo yalitarajiwa kutangazwa siku ya Jumapili ya Januari 6 lakini yakaahirishwa.

Hali ya taharuki imeendelea kutanda baada ya matokeo ya uchaguzi kucheleweshwa.


Vizuizi vya barabarani vimewekwa na polisi mbele ya ofisi za Tume ya Uchaguzi.

Wiki iliyopita,Rais wa tume hiyo, Corneille Nangaa, alidai sababu kuu ya ucheleweshwaji wa matokeo ni kutokana na kituo kikuu cha kuhesabia kura kilikuwa bado kinasubiri matokeo ya zaidi ya asilimia 80 ya kura zilizopigwa kutoka vituo mbalimbali kote nchini humo.

Alidai kuwa ilikuwa bado ni mapema mno kubaini chanzo cha kuchelewa kwa matokeo hayo, lakini vyama vya upinzani vinadai hiyo ni njama ya kuiba kura.

Bwana Nangaa, ambaye hajasema ni lini matokeo yatatangazwa ametoa wito kwa watu kuwa na subira licha ya hali ya wasiwasi inayoendelea kushuhudiwa nchini kutokana na kucheleshwa kwa matokeo ya uchaguzi.

Uchaguzi huo ulikuwa wa kumtafuta mrithi wa rais Joseph Kabila, ambaye anaachia madaraka baada ya kuongoza nchi hiyo ya maziwa makuu kwa miaka 18.

Kabila ameahidi kwamba uchaguzi huo ambao ulikuwa umepangwa ufanyike miaka miwili uliyopita utakuwa wa kwanza wa kupokezana madaraka kwa njia ya kidemokrasia nchini DR Congo tangu taifa hilo lilipojinyakulia uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.

Mrithi amtakaye ni waziri wa zamani wa mambo ya ndani Emmanuel Shadary ambaye anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wagombea wa upinzani Martin Fayulu,tajiri mkubwa wa mafuta na Felix Tshisekedi, mtoto wa kigogo wa upinzani.


Awali Kanisa Katoliki ambalo lina ushawishi mkubwa nchini DRC,
Kanisa hilo lilitoa jumla ya waangalizi 40,000 limesema kuwa linajua ni nani aliyeshinda uchaguzi.

Maaskofu wa kanisa hilo wamewataka watawala nchini humo kuwa wakweli na kutangaza matokeo hayo karibuni.

Tamko hilo limekosolewa vikali na maafisa wa serikali ya bwana Kabila.

Siku moja baada ya uchaguzi huduma ya mawasiliano ya intaneti ilifungwa katika miji muhimu ya taifa la DRC katika hatua ambayo serikali ilesema ni ya kudhibiti kusambazwa kwa matokeo ya uchaguzi amabyo sio rasmi.

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa wanajeshi 80 wa nchi hiyo wamepelekwa katika taifa jirani la Gabon ili kuwapa ulinzi raia wake nchini DRC endapo ghasia zitatokea baaada ya uchaguzi..

Waliyogombea urais ni kina nani?

Kulikuwa na jumla ya wagombea urais 21 lakini wagombea wakuu ni watatu:


Martin Fayulu, Mkurugenzi mkuu wa zamani wa mafuta ambaye ameahidi nchi yenye mafanikio lakini ambaye watu maskini wanahisi hawezi kuwatetea.

Emmanuel Ramazani Shadary, Waziri wa zamani wa mambo ya ndani na mtiifu kwa Kabila, ambaye aliwekewa vikwazo na Muungano wa Ulaya kwa hatua zilizochuliwa upinzani wakati wa maandamano ya mwaka 2017.

Felix Tshisekedi Tshilombo, Mtoto wa mwanasiasa mkongwe ambaye ameahidi kupambana na umaskini.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.