Followers

Platinum Credit[Vita Ya Mafuta]



Vita ya mafuta
Yahusisha wafanyabiashara vigogo
Kamati ya Bunge sasa ‘yagawanyika’
Wajumbe baadhi waomba waondoke

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
Mpasuko umejitokeza ndani ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Viwanda, Biashara na Mazingira; sababu kuu ikitajwa kuwa ni biashara
ya mafuta ya mawese kutoka Indonesia na Malaysia.
Hatua hiyo imewafanya baadhi ya wabunge waoneshe kusudio la
kumwomba Spika Job Ndugai, awaondoe kwenye kamati hiyo ili
kupisha kile wanachokiita kuwa ni ‘aibu’ inayoweza kuwapata endapo
wataendelea kudumu kwenye kamati hiyo.
Wajumbe hao ni wale wanaopinga madai ya kwamba mafuta ya
mawese yanayoingizwa nchini kutoka mataifa hayo ni ghafi. Wanaamini
mafuta hayo yameshachakatwa, na kwamba kinachofanywa na baadhi
ya wafanyabiashara ni ujanja-ujanja wa kukwepa kulipa ushuru na kodi
za Serikali.
Tangu Aprili, mwaka huu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezuia
meli mbili zenye shehena ya tani 62,000 za mafuta ya mawese ikitaka
wahusika walipe ushuru wa asilimia 25. TRA wanasema mafuta hayo si
ghafi, lakini wafanyabiashara wanapinga wakidai ni ghafi kwa hiyo
watozwe ushuru wa asilimia 10.
Mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni wastani wa tani za ujazo laki 4 kwa
mwaka; ilhali uzalishaji ni tani 150,000. Takwimu zinaonesha kwa miaka
mitatu (2013-2015) Tanzania ilitumia dola milioni 604 za Marekani
kuagiza mafuta ya kula, mafuta ya mawese yakiongoza.
Akiwa mkoani Singida mwezi uliopita, Rais John Magufuli aliagiza
kulindwa kwa viwanda vya ndani kwa kuhakikisha mafuta yanayotoka
nje yanayotozwa ushuru stahiki.
Tangu shehena ya mafuta hayo ilipozuiwa bandarini kumejitokeza

watetezi, baadhi wakiwa katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Viwanda, Biashara na Mazingira.
Kamati hiyo inaundwa na wabunge 26. Mwenyekiti wake ni
mfanyabiashara Mbunge wa Mvomero, Saddiq Suleiman (Murad-
[CCM]).
Baadhi ya wajumbe ni wafanyabiashara maarufu nchini. Pamoja na
Murad, wajumbe hao ni Mansoor Shanif, Salim Hassan Turky, Sylvester
Koka, Abdulaziz Abood na Mansoor Shanif.
Kuwapo kwa baadhi ya wajumbe kwenye Kamati hiyo kunaibua hisia za
mgongano wa maslahi. Unatolewa mfano wa Mbunge wa Mpendae,
Turky, ambaye ni mjumbe wa miongoni mwa viwanda vinavyosindika
mafuta ya mawese.
Turky hataki kuzungumzia ubia wake kwenye viwanda hivyo, licha ya
msimamo wake kujulikana wazi kuwa unaegemea kwa waagizaji mafuta
kutoka ughaibuni. Ameulizwa na JAMHURI, lakini amejibu kwa ufupi
kuwa yeye si msemaji wa Kamati husika ya Bunge.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na
Mazingira ni:
1. Saddiq Suleiman (Mwenyekiti)
2. Hawa Mwaifunga
3. David Mwambe
4. Balozi Dkt. Diodorus Kamala
5. Gimbi Masaba
6. Jumanne Kishimba
7. Lucy Mayenga
8. Kiteto Koshuma
9. Innocent Bashungwa
10. Munde Abdalah
11. Omary Badwel
12. Khamis Ali Vuai
13. Munira Mustafa Khatibu
14. Salim Hassan Turky

15. Shamsia Azizi Mtamba
16. Sylvester Koka
17. Ahmed Ally Salum
18. Zainab Amiri
19. Kanali (Mst.) Masoud Ali Khamis
20. Josephine Genzabuke
21. Gibson Meiseyeki
22. Godbless Lema
23. Abdulaziz Abood
24. Mussa Ntimizi
25. Ahmed Juma Ngwali
26. Mansoor Shanif
Aliyekuwa Mbunge wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya (CCM), kwenye
taarifa yake ya uchunguzi aliliambia Bunge kuwa hakuna mafuta ghafi
ya mawese yanayoletwa nchini.
Alisema utafiti aliofanya kwa kwenda katika nchi hizo ulithibitisha pasi
na shaka kuwa mafuta yanayoletwa nchini huwa tayari yamechakatwa.
Wiki iliyopita, Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa, aliagiza wafanyabiashara walioficha mafuta wawe
wameyasambaza sokoni ndani ya kipindi cha siku tatu kuanzia Alhamisi
iliyopita.
Akasema, uhaba wa mafuta ya kula nchini si jambo la bahati mbaya na
Serikali haiwezi kulikubali.
“Kuanzia Jumapili tutalazimika kuingia viwandani na kwenye maghala ili
kuhakiki kama mafuta hayapo kwa sababu kwa kufanya hilo
waheshimiwa wabunge shida tunayoipata ni sisi bila sababu yoyote.
Kuna mpango wa kuyumbisha Watanzania hasa wakati huu maandalizi
ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
“Tunahitaji kuwa na sukari ya kutosha, Serikali imeweka utaratibu
mzuri, na mafuta yapo, lakini sukari pia ipo, kama Serikali tunatoa siku
tatu kuanzia kesho Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi,” aliagiza Waziri
Mkuu.

Kwa mujibu wa Majaliwa, wastani wa matumizi ya mafuta ya kula kwa
mwezi nchini ni tani zisizozidi 28,000 lakini takwimu zilizopo zinaonesha
kuwa kila mwezi zinaingizwa tani 30,000 mafuta ya kula.
“Mafuta tuliyoagiza Januari, Februari, Machi yanafika zaidi ya tani
30,000, yalikuwa yanaweza kabisa ku-cover mwezi Aprili na mafuta ya
mwezi Mei ambayo yalipokelewa jana (Jumatano) na leo (Alhamisi)
yanaendelea kupokelewa tani 46,500 kusingekuwa na sababu ya uhaba
wa mafuta” alisema.
Kauli yake ilitanguliwa na Spika Ndugai, ambaye alishauri kuwatumia
wataalamu, ikibidi wa nje, kupima mafuta hayo ili kupata ukweli wa
kama ni mafuta ghafi, au la!
Ushauri wake umekuja baada ya kuwapo msuguano kwa Shirika la
Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA);
kwa upande mmoja dhidi ya TRA. TRA wanaamini mafuta hayo si ghafi,
lakini wafanyabiashara wanadai ripoti ya TBS na TFDA inathibitisha
pasi na shaka kuwa shehena yao ni ghafi.
Mei 8, mwaka huu Spika Ndugai alimtaka Waziri wa Viwanda, Biashara
na Uwekezaji, Charles Mwijage, kufikia saa 11 jioni ya siku hiyo
kuwasilisha bungeni taarifa ya kinachoendelea kuhusu mafuta ya kula.
Ndugai alitoa kauli hiyo wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa Nzega
Mjini, Hussein Bashe (CCM), aliyehoji bei ya mafuta, akisema
imepanda.
Chanzo cha habari kutoka serikalini kimesema Rais Magufuli ameingilia
kati sakata hilo, na ameagiza mamlaka za nchi zipime na kutoa majibu
kuhusu mafuta hayo yaliyokwama bandarini ambayo TRA inataka ilipwe
ushuru wa shilingi zaidi ya bilioni 20.
Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, waagizaji walikuwa hawajawasilisha
TRA nyaraka halisi zenye maelezo yanayopambanua uhalisia wa
mafuta hayo kutoka katika nchi yalikoagizwa.
Hata hivyo, JAMHURI limedokezwa kuwa Indonesia na Malaysia
hawaruhusu kusafirishwa nje ya nchi mafuta ghafi, wakiamini kwa
kufanya hivyo kunasaidia kuongeza thamani na ajira kwa wananchi
wake.
“Mafuta ya mawese yanayosemekana kuwa ghafi kutoka nje yana
‘acidity level’ yaani ‘free fatty acid’ (ffa) ya chini sana kulinganisha na
‘crude’ halisi. Hiyo ni ishara kwamba yalichakatwa kabla kuingia nchini,”
kimesema chanzo chetu.

Unatolewa mfano kuwa mafuta ghafi halisi yaliyokamuliwa kutoka
michikichi iliyopo Kyela, kwa mfano yamepimwa na TBS na kukutwa na
kiwango cha ‘acidity level’ ya asilimia 14.
Mmoja wa maofisa ‘wazalendo’ waliopo TBS anasema ili kumaliza
ubishi uliopo, anashauri ichukuliwe michikichi kutoka Malaysia na
Indonesia, ipimwe kuona kama kuna tofauti ya ‘acidity’ na michikichi ya
hapa nchini.
Shaka nyingine, anasema, kwenye kiasi cha ‘ffa’ kinachotumiwa na
TBS kwenye mafuta ghafi ambako ni asilimia 0.6 hadi kiwango cha juu
cha asilimia 10. Kwa kiwango hicho mafuta hukubalika kuwa ni ghafi.
“Hapa TBS tumekuwa tunajiuliza, kama kiwango hicho cha asilimia 10
ndicho cha juu; je, kiwango cha asilimia 14 ffa kitawekwa kundi gani?”
Anahoji.
Mfanyabiashara mmoja aliyeshiriki biashara hiyo kabla ya kuiacha,
anasema mafuta ya mawese yanayoingizwa Tanzania na Afrika kwa
ujumla yanatoka kwenye magenge ya wafanyabiashara nchini Malaysia
na wenzao nje ya nchi hiyo.
“Huwezi kusafirisha mafuta ghafi kutoka Indonesia au Malaysia. Huwezi
kuruhusiwa. Haya mafuta ni refined asilimia 100 tayari kwa kutumiwa.
Wanachofanya kule wanakoyatoa wanaweka mafuta safi kwenye meli
halafu wanachanganya asilimia 1 au 2 ya ffa na rangi nyekundu.
“Nitakupa mfano, chupa ya maji ya kunywa ukichanganya tone moja la
wino, maji yataonekana machafu au ‘crude’. Ndiyo maana wanachakata
mafuta haya hapa nchini kuondoa ‘ffa’ na wino (rangi) walioweka na
kisha wanajaza mafuta kwenye vyombo tayari kuyauza. Wanachofanya
siyo ‘refining’ bali ni filterization’.
Mkurugenzi wa TRA wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard
Kayombo, amezunguma na JAMHURI na kusema taarifa zilizopo ni
kuwa mafuta yanayoingizwa nchini si ghafi.
“Tumeomba walete proof [uthibitisho], hawajaleta. Tumewataka walipe
ushuru [to pay under protest] ili endapo itathibitika kuwa mafuta ni ghafi,
basi taratibu nyingine za kisheria zifuatwe – kama kwenda kwenye
tribunal [kwenye usuluhishi],” amesema Kayombo.
Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere, ameliambia JAMHURI kuwa
taratibu za kupata ukweli kuhusu mafuta hayo zinaendelea.
“Tunachojua ni kuwa Malaysia na Indonesia wana-discourage
kusafirisha nje ya nchi hizo ‘crude oil’, ni kama sisi tunavyofanya

kwenye korosho na mazao mengine.
“Hili suala linashughulikiwa kwenye vyombo husika vya kitaalamu,”
amesema Kichere.
Kwa upande wake, Murad aliahidi kuzungumza na JAMHURI lakini hadi
tunakwenda mitamboni hakuweza kutoa kauli yoyote.
Ushuru kwenye mafuta ya kula ya mawese ulifutwa na aliyekuwa Waziri
wa Fedha na Uchumi, kupitia hotuba yake aliyowasilisha bungeni ya
Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi
kwa mwaka wa Fedha wa 2009/2010.
Uamuzi wa Mustafa Mkulo ulikuwa tofauti na wa mtangulizi wake, Zakia
Meghji, ambaye aliweka ushuru kama njia ya kulinda viwanda vya ndani
na kuleta tija kwa wakulima.
Wakati fulani Meghji alinukuliwa akilalamikia shinikizo kubwa la
wafanyabiashara waliokuwa tayari kufanya waliloweza ili ushuru huo
usiwepo; lakini akashinda vishawishi hivyo.
Mkulo kwenye hotuba yake wakati akifuta ushuru, alisema: “Tanzania
kuondoa Ushuru wa Forodha wa asilimia 10 unaotozwa kwenye mafuta
ghafi ya kula ya mawese (Crude Palm Oil) na kutoza asilimia sifuri
kama ilivyo kwa nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Alisema hatua hiyo ililenga kuviweka viwanda vya mafuta vya hapa
nchini katika nafasi nzuri kiushindani na vya wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo, Mkulo alipingwa na baadhi ya wabunge kwa maelezo kuwa
hakuna ushindani wa viwanda vya mafuta katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Mizengwe kilimo cha michikichi
Ripoti ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) ya mwaka 2014/2015 ilibainisha mizengwe inayozuia
uanzishwaji wa mashamba na viwanda vya kusindika mafuta ya
mawese nchini.
Ingawa hakutaja sababu za urasimu, duru za uchunguzi zilionesha
kuwa mkwamo huo unasababishwa na mtandao wa wafanyabiashara
waagizaji wa mafuta ya mawese.
Mradi uliokwamisha wa uzalishaji mafuta ya mawese ulikuwa wa ubia
kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya NAVA

Bharat Singapore PTY Ltd. Ununuzi wa ardhi ya ukubwa wa hekta
10,000 ulitarajiwa kufanywa na NDC.
Ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mafuta ya mawese na uzalishaji wa
megawati 10 za umeme wa mimea ulitazamiwa kufanywa na mbia
binafsi, ambako kwa ujumla wake kungepatikana lita milioni 58 za
mafuta ya mawese.
Hata hivyo, hadi ukaguzi wa CAG unakamilika, mradi huo ulikuwa
haujaanza kwa kile alichosema ni urasimu uliodumu kwa miaka mitatu.
CAG alisema: “Barua ya Desemba 6, 2015 yenye kumbukumbu namba
KSW/130/Vol III/1 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kwenda
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliyohusu ombi la
kuhamisha ardhi yenye ukubwa wa hekta 4,000 (kati ya hekta 10,000
zinazohitajika) katika eneo la Kijiji cha Kimala Misale kwenda Shirika la
Maendeleo la Taifa, ilichukuwa mwaka mzima kwa barua hii kujibiwa
kwa mradi husika kukubaliwa na maombi hayo kupelekwa rasmi kwa
Ofisi ya Rais kwa barua yenye kumbukumbu namba LD/314579/21 kwa
uthibitisho wa mwisho.
“Sambamba na hilo, Shirika (NDC) lilipokea barua yenye kumbukumbu
Na. CEA 110/302/V/01/32 ya Desemba 29, 2015 kutoka Ofisi ya Rais
ikilitaarifu kwamba barua imetumwa Halmashauri ya Wilaya ya
Kisarawe ili kupata taarifa sahihi kabla ardhi haijamilikishwa kwa mmiliki
mpya kwa mujibu wa kifungu namba 114 (1) cha Sheria ya Ardhi na
Vijiji inayoruhusu umilikishaji ardhi ya kijiji kwa matumizi ya umma.
“Karibu miaka mitatu imepita, lakini Shirika bado halijapata uthibitisho
wa umiliki wa ardhi ya ukubwa wa hekta 4,000 liliyoomba hivyo
kuongeza sintofahamu kwenye utekelezaji wa mradi.
“Taratibu za uombaji wa ardhi ya nyongeza ya hekta 6,000 katika vijiji
vya Dutumu na Madege haziwezi kuanza bila ombi lililopita la hekta
4,000 kufanyiwa kazi ikiwamo ulipwaji wa fidia kwa wamiliki husika.”
Kukwama kwa mradi huo kunaelezwa kusababishwa na vita kati ya
wazalishaji walioko Indonesia na Malaysia kwa upande mmoja; dhidi ya
mwekezaji kutoka Singapore aliyetaka kushirikiana na NDC.
Kunatolewa mfano wa kilimo cha mawese kilivyokufa nchini Nigeria,
chanzo kikuu ni vita ya wakulima wa mataifa yanayolima mawese na
wafanyabiashara dhidi ya wale walioamua kuwekeza kwenye kilimo na
kufungua viwanda nchini Nigeria.
“Haya yatatokea hata hapa kwetu, Indonesia na Malaysia hawatakubali

tuanzishe mashamba makubwa ya michikichi. Wanataka tuendelee
kuwa soko lao… vita hii ni kubwa kama ya sukari au hata zaidi,”
kimesema chanzo chetu.

No comments

Theme images by sandoclr. Powered by Blogger.