Wananchi wamuona Mkuu wao wa Wilaya baada ya kupita miaka nane
Wananchi katika kijiji cha Maperamengi wilayani Iringa, wamefurahia ziara ya kwanza ya mkuu wa wilaya hiyo Richard Kasesela baada ya kupita miaka 8 tangu alipowatembelea aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo mwaka 2010.
Wakiongea katika mkutano wa hadhara, wanakijiji walieleza kiu yao ya kutaka kutatuliwa kwa kero zao lakini hawakuwahi kupata sehemu sahihi ya kueleza kero hizo kwa muda wa miaka 8.
“Kijiji chetu mara ya mwisho kumpokea Mkuu wa wilaya ilikuwa 2010, ambapo Mkuu wa wilaya alikuwa Msangi na kuanzia hapo hakuna mkuu yoyote aliyewahi kufika hapa hivyo ujio wako tunaamini utatatua kero zetu nyingi“ alieleza mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Marwa.
Moja ya kero kubwa zilizotajwa na wananchi wa Maperamengi ni uwepo wa wanyama hatari kama Viboko katika ziwa Nyasa kwenye eneo la karibu na kijiji hicho ambapo wanyama hao wamekua wanaua wavuvi hivyo wameshauri serikali ivune wanyama hao ili wapungue.
Mh. Kasesela ameahidi kushughulikia kero tofauti tofauti kijijini hapo ambapo baadhi yake ameanza kwa kukagua ujenzi wa darasa ambalo mpango wa ujenzi wake aliuanzisha mwenyewe mwaka jana kwa kuchangisha fedha na sasa amejionea ujenzi unavyoendelea.
No comments
Post a Comment